Wednesday, July 1, 2020

Kuna hatari taasisi za Watanzania ughaibuni kuingiliwa na mchwa

NA TENGO KILUMANGA

KUANDIKA kichwa habari cha namna hii si kwamba natafuta makosa au natafuta njia ya kuwakosoa baadhi ya viongozi ughaibuni la hasha, lakini najaribu kutafuta njia za kuangalia ndani ya changamoto hizo ambazo tusipozijadili na tusipozikubali basi hata ile nia ya nguvu ya kutaka kusaidia nyumbani inaweza kupotea.

Warren Bennis, katika utafiti wa uongozi, anasema  “Uongozi ni uwezo wa kutafasiri maono kuwa ukweli,” na kukuza mabadiliko kwa njia bora kwa hiyo lazima uwe na uwezo wa kutatua maadili na vipaumbele vya kutatanisha katika jamii. 

Kiongozi lazima awe na uwezo wa kutazama picha kubwa, kuangalia mambo yote ambayo yanaathiri jamii anayoiongoza na kupitisha kuwa maono na kutenda kitendo cha kuiongoza.

Kuwaunganisha Watanzania ughaibuni si kazi rahisi, ingawa tuna lugha moja ya Kiswahili lakini bado changamoto ni nyingi sana. Watanzania tunatoka kwenye mazingira tofauti, tumepishana sana kwa umri halafu kuna wale ambao wapo ughaibuni miaka mingi. Kuna Watanzania wa enzi za Mwalimu Nyerere, wapo ambao wamelelewa kwenye miaka ya analogi na simu za kukoroga, wengine kwenye miaka ya  ‘dot com’ na mitandao ya kijami. 

Kwenye mazingira hayo hayo tunaigiza sasa BC na AC, yaani ‘before Covid-19’(kabla ya Covid-19) na ‘after Covid-19’ (baada ya Covid-19) ambapo tunaelekea.

Kuishi nje ya Tanzania na kupata mabadiliko mengi ambayo hufanyika, kiuchumi, kijamii na kisiasa moja kwa moja au kwa njia moja kwa moja kuathiri maisha katika jamii inalazimisha uongozi wa sasa kukuza uwezo wa kuchukua, kuzoea na kushughulikia maendeleo. 

Kama kiongozi, unapaswa kuwa na uwezo wa kushawishi kwa kukusudia jamii kuunga mkono kuandamana kuelekea lengo moja kabisa. Sehemu mbaya zaidi ikiwa inatumiwa kwa faida za kibinafsi.

Kuongoza Watanzania ambao wana elimu inayopishana na pia tunapishana sana kwenye maono. Ukiweka nchi wanazoishi na tamaduni za hapo walipo hakuna urahisi kwenye kuwaunganisha Watanzania ni kazi kubwa sana. Ni kusema kwamba Watanzania ni kama mfupa wa fisi. Ni wapole, wataratibu na wana heshima sana lakini ukiwatibua ni watu ambao hawatakuachia. 

Nafikiri Watanzania wengine ni baadhi ya wale waliopigwa ule msasa wakiwapo mashuleni enzi za Mwalimu, au waliopitia jeshini. Kwa ujumla Watanzania ughaibuni wanaipenda sana nchi yao, wanapenda utamaduni wao na wanajitahidi sana kuwa karibu na Watanzania wenzao. 

Lakini  kama kiongozi kwenye jumuiya ya Watanzania ughaibuni usiwakorofishe.

Jumuiya ya Watanzania duniani ambayo imesajiliwa Sweden imeingiliwa na mchwa kwenye msingi na nguzo zake kuna matatizo ambayo ni ya maono ya utendaji.

Katika kila ujenzi wa nyumba yoyote ile lazima kuwe na msingi mzuri, kinga nzuri na kuangalia nyumba inajengwa kwenye mazingira gani. Na msingi mzuri unaletwa na utafiti mzuri na ustamilivu. Sio rahisi kama watu wanavyofikiria. Sio nyumba tu hata kwenye ujenzi wa jumuiya. 

Mlezi ni kitu muhimu sana katika ujenzi wa jumuiya, mlezi ni kama kumbukumbu ya makumbukumbu. Anatoa ushauri kutokana na hekima, busara, uzoefu na ujuzi aliokuwa nao. 

Kwenye nyumba kupata mchwa ni lazima kuwe na mazingira fulani na hasa kwa mwenye nyumba ambaye hajali nyumba yake. Mchwa wanastawi kwenye mazingira ambayo hayana uhai na hasa kwenye sehemu za mbaombao na miti mikavumikavu. Ukimwangalia mchwa ni mdudu mdogo sana, usidanganywe na udogo wake, mchwa wana meno makali sana na utashangaa jinsi anavyo kula misingi ya mbao ya nyumba bila mwenye nyumba kuona na kuelewa kinachoendelea. Ni mdudu hatari sana na anasababisha athari kubwa sana usipomzuia na kumwondoa. 

Ni kama kwenye kuunda au kujenga Taasisi, Jumuiya au hata nchi, utapata tu watu ambao wana tabia za kimchwa. Na wanapenda mazingira ambayo msingi wake ni dhaifu na hakuna uongozi au kinga ambayo inaeleweka. Watu kama hao wanatafuna jumuiya kwa ndani na kuimaliza. 

Ni rahisi kuingiza tabia za kimchwa ambaye anaishi kwa kula mimea na mbao ambazo zimekauka na hazina maisha. Changamoto inakuja kwenye kiongozi ambaye ana maono mengine tofauti na yale malengo na kanuni ambazo zipo kwenye chombo ambacho ameombwa na kukabidhiwa kukisimamia. 

Kinga moja nzuri sana ni kuwa na uongozi bora ambao unaona mbali na hapo hapo kuwa na katiba ambayo inalindwa na miongozo na utaratibu mzuri wa kiutendaji. Katiba ni karatasi tu ambalo linaandikwa na binadamu kama wengine na kunaweza kuwepo makosa. Kuongoza jamii hivyo katika muundo wake, iliopo katika viwango tofauti vya kijiografia na tofauti na wakati huo huo maisha ni katika jamii yenye ushawishi mkubwa sana wa kijamii sio kazi rahisi na kinga ya kuepuka mchwa ni kunahitajika umakini mkubwa sana. 

Uzoefu wa watu ambao wanaweza kuongoza na kusimamia inaleta nguzo nyingine katika ujengaji wa jumuiya ya sasa na baadaye. Uwezo wa kuweza kusoma alama za nyakati na kuelewa kwamba kunahitajika marekebisho na uelimishaji wa jamii ambao unawaongoza na hapo suala la mlezi ni muhimu kwa kuweza kushauri bila kufungamana na upande wowote. Kutoa mwongozo pale ambapo pana mapungufu bila ya kutoa hukumu wakati huohuo. 

Ukimuwahi mchwa na kuweka kinga basi hakika nyumba itakuwa mahali pema ila kinga wakati wote lazima iwe karibu na utendaji na taratibu zinafuatwa wakati wote. Uongozi uliochanguliwa na watu na wakaungwa mkono nao ni rahisi kujenga kinga nao kwa pamoja kutaka kuwatumikia ni malengo mazuri. Hapa nazungumzia sana kuhusu jumuiya ya kujitolea, kufanya kazi ya kujitolea ni wito na hauna masilahi binafsi. Upande mwingine ung’ang’nivu wa kusema juu ya msimamo au uzoefu bila ufahamu ni dhahiri utaathiri wengine ni vitendo vya ubinafsi, hii haisaidii jamii na uwepo wake ni wa muda mfupi.

Tusikubali mchwa wakaingia mpaka ndani ya nafsi yetu tukaanza kujenga tabia za kimchwa. Ukishasikia hilo ni kutekeleza tu.

Kwa upande mwingine mchwa ni mtengamano muhimu sana, huvunja zile nyuzi ngumu za mimea, kuchakata miti iliyokufa na kuoka ndani ya udongo mpya wa maisha. Wadudu wenye njaa ni muhimu kwa afya ya misitu yetu. Wanapochimba chini kwa chini kwenye udongo, mchwa pia husaidia kuboresha ardhi. Labda ndio dunia mpya hiyo kama Covid-19 inavyotupeleka mbio..

Na Tengo Kilumanga tel: +46705263303

instagram: @tengognet  twitter: @tengo_k  mailto: tengok@gmail.com